Watoto wawili wafariki baada ya kuangukiwa na nyumba


Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia mkoani Singida baada ya kuangukiwa na nyumba ya udongo maarufu kama tembe walimokuwa wamelala wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha.
Tukio hilo la maafa limetokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo Jumatano katika Kijiji cha Mningaa/Mkwese Wilaya ya Manyoni mkoani humo na kusababisha vifo vya watoto hao wa kiume wenye umri wa miaka 4 na 12 waliokuwa wamelala peke yao kwenye nyumba hiyo ya tembe.
Simuzi ya kusikitisha kutoka kwa familia iliyopoteza watoto wanne msimu wa mvua uliopita baada ya kuangukiwa na nyumba ya tembe katika Kijiji cha Nduguti Wilaya ya Mkalama mkoani Singida.
Wakati hali ikiwa shwari katika Wilaya hiyo iliyopata maaafa ya zaidi ya watu 10 mwaka jana kabla ya kuanzisha mpango wa Ondoa tembe, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Thobias Sedoyeka anasema mambo yamekuwa tofauti mwaka huu ambapo watoto wawili wamekufa Wilayani Manyoni.
Anasema juhudi za wazazi kujaribu kuokoa maisha ya watoto hao hazikuweza kuzaa matunda.
Ingawa wito wa Polisi ni kulala jirani na watoto ili kurahisisha uokoaji, lakini baadhi ya wazazi na walezi wanasema njia pekee ni kuondoka kabisa nyumba za tembe, suala ambalo linatatizwa na bei kubwa ya vifaa vya ujenzi isiyokwenda sanjari na bei ya mazao ya biashara wanayozalisha.
 Tembe ni nyumba za asili ambazo hujengwa kwa tofali mbichi za udongo na kuezekwa kwa miti kisha kufukiwa udongo juu yake na zimekuwa zikikaliwa na wenyeji wa mkoa ya Singida na Dodoma tangu enzi za mababu, kabla ya miaka ya hivi karibuni kuanza kuporomoka kwa mvua zisizotabirika na kuleta maafa.

wdcfawqafwef