Magufuli ni kazi tu



RAIS John Magufuli ameeleza muongozo wa Serikali ya Awamu ya Tano, huku akisema amejipa kazi ya kutumbua jibu, ambalo anajua kuwa utumbuaji huo unauma, lakini hana namna. Akielezea sababu ya kujipa jukumu hilo, Dk Magufuli alianza kwa kuelezea mambo aliyolalamikiwa na wananchi wakati alipokuwa akifanya kampeni, ambapo alitumia barabara kuzungukia wananchi nchi nzima.
Alisema wakati wa kampeni, alilalamikiwa sana na masuala mbalimbali hasa rushwa na ufisadi ambao wananchi walionesha hisia zao namna wanavyochukia kwa kulalamikiwa maeneo yote yanayogusa wananchi.
Maeneo ya rushwa, kero Akianza kutaja sekta na ofisi zilizolalamikiwa, Dk Magufuli alisema ni pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambako alisema kumekuwa na malalamiko ya ubadhirifu na uchelewaji katika utekelezaji wa miradi au miradi kuwa ya viwango vya chini. Mbali na Tamisemi, alitaja pia sekta ya ardhi kuwa imekuwa na migogoro baina ya wakulima na wafugaji na sehemu nyingine kumeonekana udhaifu katika mipango miji, huku baadhi ya watu wakitumia fedha kujenga katika maeneo ya wazi.
Dk Magufuli aliendelea kutaja maeneo hayo na baada ya ardhi akahamia Bandari, ambako alisema imetajwa kuwa na vitendo vya rushwa na wizi na kutaka watendaji wake wafanye kazi kwa pamoja ili kuondoa malalamiko hayo. Kero nyingine aliyolalamikiwa, alisema ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, kwamba vyanzo vyake vimekuwa mbali na makazi ya wananchi na kuongeza kuwa kazi ya Serikali itakuwa kuwatua wanawake ndoo kichwani.
Mbali na kukosekana kwa maji, Dk Magufuli alitaja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akasema imelalamikiwa na ukwepaji wa kodi kwa wafanyabiashara wakubwa, urasimu na ubadhirifu. Ukiacha malalamiko hayo ya TRA, Dk Magufuli alisema malalamiko mengine ya wananchi ni katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na yalihusu kero ya kukatika kwa umeme pamoja na mgawo wa mara kwa mara.
Sekta nyingine iliyotajwa kuwa kero kwa mujibu wa Dk Magufuli, ni maliasili na utalii na malalamiko yake yamejikita katika ujangili, suala alilosema kuwa watendaji wa sekta hiyo wanahusika, kwani meno ya tembo, hayawezi kushikiliwa katika nchi za Ulaya bila wahusika kufahamu pamoja na upotevu wa mapato na migogoro ya mipaka. Rais alisema malalamiko mengine ni huduma za afya kuwa mbali na wananchi, kutopatikana kwa dawa na huduma za vipimo, vitendea kazi, rasilimali fedha na watu pamoja na lugha mbaya kwa wafanyakazi wa sekta ya afya.
Pia wananchi wamemlalamikia kuhusu Idara ya Uhamiaji na utoaji uraia, kwamba kumekuwa na utaoaji hati na vibali vya kufanya kazi kwa wageni bila kufuata utaratibu na utoaji vibali vya ajira kwa wageni kwa kazi zinazofanywa na Watanzania. Katika suala la elimu, alisema kumekuwa na malalamiko ya michango mingi, maslahi madogo ya walimu, ukosefu wa miundombinu na nyumba za walimu na masuala mengine ya utoaji elimu kutopatikana.
Alisema pia Jeshi la Polisi limelalamikiwa kwa kubambikiza kesi wananchi, kutoa upendeleo kwa walalamikaji, askari kutotimiziwa haki zao na Jeshi la Zimamoto kuchelewa katika matukio na wakati mwingine kufika bila maji ya kutosha.
Mizani pia imetajwa katika kero kwa wananchi, kwamba imekuwa ikichelewesha magari yanayosafirisha bidhaa nje ya nchi, kwa lengo la kupata rushwa, huku Idara ya Mahakama ikilalamikiwa kwa uchelewaji wa kesi. Katika sekta ya madini, Dk Magufuli alisema wananchi walilalamika kutofaidisha wenyeji, kukosekana kwa mikopo kwa wachimbaji wadogo, ukwepaji kodi na kulipwa fidia kwa wananchi.
Kwa upande wa kilimo na ufugaji, Dk Magufuli alisema kilio kikubwa ni malalamiko ya kukopwa mazao yao, kukosekana masoko na wataalamu, kukosekana malambo na majosho, huku uvuvi wakilalamikia vifaa duni, kukosekana masoko na viwanda huku nchi ikiwa na ukanda wa bahari wenye urefu wa kilimeta 1,422.
Shirika la Reli nalo halikuachwa, ambapo Dk Magufuli alisema limelalamikiwa kwa kuwa na miundombinu chakavu, huku Shirika la Ndege Tanzania (ATC), likiwa na wafanyakazi wengi wanaohangaika na ndege moja tu.
Kuhusu makundi maalumu, Dk Magufuli alisema kuna malalamiko ya haki za wazee, walemavu, wanawake na watoto pamoja na kodi za wafanyakazi kuwa kubwa ikiwemo ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE), hivyo ni lazima Serikali ijipange kushughulikia na kutatua kero kwa kushirikiana na Bunge.
Kazi iliyo mbele Baada ya kuorodhesha kero hizo, Dk Magufuli alisema kazi atakazofanya na mambo atakayosimamia, ni pamoja na udhibiti wa matumizi ya fedha serikalini kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Dk Magufuli amesema ataunda Serikali ndogo huku akionya watumishi wazembe akisema wajiandae kwani wakati wa kuchezea na kuchakachua Watanzania umekwisha na habari za michakato inayoendelea kwenye kazi serikalini vitakoma kwani wapo wanaolipwa mishahara, lakini hawafanyi kazi na kufanya serikalini kuwa eneo la kuchuma.
Katika kuongeza mapato na kupunguza matumizi ya Serikali, Dk Magufuli alisema kwa miaka mitatu iliyopita, ukusanyaji mapato uumekuwa chini ya makadirio kutokana na wakwepa kodi hivyo sasa atawachukulia hatua na kuhakikisha kila anayenunua bidhaa anapewa risiti.
Dk Magufuli amesema ataziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali kwa kuanza na kupunguza safari za watumishi zisizo na lazima nje ya nchi na badala yake atatumia mabalozi na akilazimika, kiongozi hatakwenda na misururu ya watu.
Gharama safari za nje Akitoa mfano namna safari hizo zilivyokuwa zikila fedha, Dk Magufuli alisema zaidi ya Sh bilioni 356.3 zilitumika kwa safari za nje, ambapo tiketi za ndege ilikuwa Sh bilioni 183.16, mafunzo ya nje Sh bilioni 68.62 na posho za kujikimu Sh bilioni 104.552.
Alisema Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Wizara ya Mambo ya Ndani, ndiyo zinaongoza kwa matumizi ya fedha nyingi za safari za nje, wakati fedha hizo zingetumika kuboresha maisha ya Watanzania na zingeweza kutengeneza barabara ya kilometa 400.
Aliwaomba wabunge kumsaidia katika kudhibiti matumizi, kwani suala kama la mafunzo, badala ya kundi la watumishi kwenda nje ya nchi, wangeweza kumleta mwalimu nchini na kupata mafunzo husika.
“Hatuwezi kutatua matatizo yaliyopo kwa kuendelea kuwa na matumizi ya hovyo, kuna mtu kasafiri nje ya nchi kuliko alivyokwenda kumsalimia mama yake,” alisema na kufanya wabunge kuangua kicheko.
Alisema pia katika kudhibiti matumizi, atadhibiti semina, warsha na makondamano yasiyo na tija, kwani siku hizi wizarani lazima wakutane hotelini hata kama kuna ukumbi wakati suala lenyewe, hata kwenye mti wanaweza kukutana na kulijadili.
Akizungumzia Sheria ya Manunuzi, Dk Magufuli alisema ni mdudu mwingine mbaya kwani nyumba inayojengwa kwa Sh milioni 30 kwa sheria hiyo itajengwa kwa Sh milioni 200 au peni ya Sh 1,000, itanunuliwa kwa Sh 10,000. Alisema sheria hiyo ni mbaya katika kudhibiti matumizi ya Serikali na kuwataka wabunge kumuunga mkono wakati muswada wa marekebisho ya sheria utakapopelekwa bungeni. Rushwa Dk Magufuli alisema atapambana bila kigugumizi dhidi ya vitendo vya rushwa kwani dawa ya jipu ni kutumbua na anajipa kazi hiyo ya kutumbua majipu ingawa anajua kuna maumivu lakini hakuna dawa nyingine.
“Naomba mniombee wakati nikitumbua majipu, nawaomba na wabunge mniunge mkono kwani najua changamoto na ugumu wa kutumbua majipu kwani wanaojihusisha na vitendo hivi, ni wakubwa wenye dhamana ya utumishi walioomba ridhaa kwa wananchi,” alisisitiza.
Alisema kutokana na dhamira yake hiyo, ameamua kuunda Mahakama ya ya Rushwa na Ufisadi na kutaka vyombo vinavyohusika kumuunga mkono.
Dk Magufuli pia alitoa onyo kwa viongozi atakaowateua, kukumbuka kwamba anayo mamlaka ya kuwawajibisha akibaini wanajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, kwani atawatimua mara moja na baada ya hapo hatua za kisheria zitafuata.
Alisema Watanzania wana maisha ya chini na wameshindwa kunufaika na rasiliamli zao, wakati nchi yao ni tajiri hivyo Serikali itafuatilia mienendo ya watendaji wake na wakibainika kuwa na vitendo hivyo, watachukua hatua katika ngazi zote.
Katiba mpya, madini Kuhusu Katiba mpya, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekuta kiporo cha katiba ambacho hakikukamilika kuandikwa, kutokana na kuchelewa kwa suala la kuandikishwa wapigakura na kwa kuthamini haki ya wananchi waliotoa maoni yao ya katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge la Katiba, serikali yake itatekeleza wajibu wake.
Rais Magufuli pia alizungumzia kuimarisha misingi imara ya kiuchumi kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za mikoa, wilaya na katika ameneo muhimu. Alisema uboreshaji wa barabara, bandari utafanyika pamoja na ujenzi wa reli mpya kwa kiwnago cha kimataifa kutoka Dar es Salaam- Tabora-Kigoma hadi Mwanza na Uvinza –Burundi, Mtwara-Songea- Bambabay na kwingineko.
Akizungumzia suala la madini, maliasili na gesi asilia, alisema yatatumika kwa manufaa ya Taifa kwa kuzingatia sheria na taratibu huku akipongeza Sheria Mpya ya Usimamizi wa Mapato ya Gesi iliyopitishwa na Bunge la 10.

wdcfawqafwef