Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amezungumzia kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM, akifananisha kushindwa kwake na kifo cha ghafla.
Akizungumza jana kwenye kongamano la
Diaspora, Membe ambaye alivuka hatua ya awali ya mchujo akiwa mmoja wa
watu watano ambao majina yao yalipelekwa kwenye kikao cha Halmashauri
Kuu ya CCM, alishika nafasi ya mwisho kwenye kura akiwa nyuma ya Dk John
Magufuli, Balozi Amina Salum Ali, Dk Asha-Rose Migiro na January
Makamba.
Tangu ashindwe kwenye kura hizo mapema mwezi
uliopita, waziri huyo hakuwahi kuzungumzia kuanguka kwake, lakini jana
aliweka bayana hisia zake.
“Kwenye mpira unaweza kupata timu nzuri sana inacheza kwenye ligi, ikafanya vizuri,” alisema.
“Lakini
mwishoni inapotoka droo (sare) na timu nyingine, timu zinakwenda kwenye
penalti. Sasa inaweza kutokea ikafungwa penalti zote tano na timu
nyingine ambayo wewe hukutegemea ikashinda vizuri tu.
“Kwenye
lugha ya kimichezo, kile kitendo cha timu iliyocheza vizuri ikashindwa
kwenye penalti, maana yake inakufa kifo kinachojulikana kama sudden
death (kifo cha ghafla). Inapopata sudden death, huitegemei isimame na
kueleza kilichotokea.”
Membe alikuwa anaonekana kuwa
mmoja wa makada waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kupeperusha
bendera ya CCM kwenye urais, lakini alianguka vibaya kwenye kura za
wajumbe wa Halmashauri Kuu.
Kuhusu kongamano hilo la
siku tatu alilofungua kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, alisema licha ya
kuwa anakaribia kuondoka madarakani atahakikisha anaendelea kupambana
ili Watanzania wanaoishi nje wapate uraia wa nchi mbili.
“Ndipo
tutakapopata maendeleo ya kweli ya wanadiaspora. Wanadiaspora watakuwa
na kazi nzuri watakapokuwa nchi za nje na watakuwa wanaingiza mabilioni
ya fedha nchini kama ilivyo kwa Kenya na Nigeria,” alisema.
Alisema
hivi sasa Watanzania hao wanashindwa kusafirisha fedha zao kwa wingi
nchini kwa sababu wengi wao ‘wamejilipua’ kwa hiyo wanazituma kinyemela,
lakini pale watakapopata fedha wakiwa na uraia wa nchi mbili, wataweza
kutuma bila kuficha.
“Natoka huku nikiendelea kuamini
kwamba diaspora ya kweli ya Tanzania na isiyo na woga wowote ni pale
watakapopata pesa za kufurahia uraia wa nchi mbili,” alisema.